Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kitakuwa na mahafali ya 42 tarehe 27 Oktoba 2012 na Novemba 3, 3012.
Jumla
ya wahitimu 3,643 watatunukiwa shahada na stashahada wakati wahitimu
902 wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ardhi (UCLAS) watatunukiwa shahada.
UCLAS kwa sasa ni sehemu ya UDSM.
Hayo yalisemwa na Makamu Mkuu wa wa UDSM, Profesa Rwekaza Mukandala akitoa taarifa kwa umma kupitia waandishi wa habari.
“Tunapenda
kuufahamisha umma pia kuwa, katika mahafali ya sasa wanafunzi wa UCLAS
na wao watatunukiwa shahada kama wanafunzi wa UDSM, uamuzi huu umefuatia
kumalizika kwa kesi Lello & Others Vs Ardhi University, University
of Dar es Salaam and Attornry General, Misc.Civil Cause No. 69 of 2008,
iliyofunguliwa na wanafunzi wa UCLAS wakipinga kupata shahada za UCLAS
kwa madai kuwa udahili wao ulibaki wa UDSM, hivyo UDSM kinakubalina kwa
dhati na uamuzi wa Mahakama Kuu,” alisema Prof Mukandala.
UDSM
imekubali kuwatunuku shahada mbalimbali wahitimu hao 902 waliomaliza
masomo yao UCLAS ambao awali waligoma kutunukiwa shahada zao na chuo
hicho (UCLAS) katika Mahafali ya 42 kutokana na madai kuwa walipata
udahili chini ya UDSM wakati UCLAS kilipopata hadhi ya kuwa chuo kikuu
kinachojitegemea mwaka 2007 hivyo walistahili kutunukiwa shahada na chuo
kilichowadahili. Wanafunzi hao ni wale waliohitimu masomo katika miaka
ya 2007 hadi 2010.
Wanafunzi hao kwa kupinga suala hilo
walifungua kesi mahakamani dhidi ya Chuo Kikuu cha Ardhi, Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
“Sisi
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam tumekubaliana kwa dhati na uamuzi huu wa
mahakama na tumeamua kuwatunuku shahada wanafunzi hao kwa vile hakuna
rufaa iliyokatwa dhidi ya uamuzi huo,” alisema Profesa Mukandala.
Kati
ya watakaotunukiwa shahada mbalimbali, 28 watatunukiwa Shahada za
Uzamivu, 671 Shahada ya Uzamili; 153 Stashahada za Uzamili na 2,
790 Shahada ya Kwanza.
Licha
ya mahafali hayo, Profesa Mukandala alisema chuo hicho kitahitimisha
maadhimisho ya miaka 50 ya kuanzishwa kwake kwa kufanya shughuli
mbalimbali ikiwamo kufanya mkutano na wahitimu waliowahi kusoma chuoni
hapo shughuli ambayo itafanyika Alhamisi.
Profesa
Mukandala alisema wakati wa kuhitimisha sherehe hizo, shughuli
zitakazofanyika ni kuweka jiwe la msingi la jengo la kituo cha
wanafunzi, kuzindua Dira ya Chuo hicho (UDSM Vision 2061) na kutoa tuzo
mbalimbali kwa watu na vikundi vilivyotoa mchango uliotukuka kwa chuo
kikuu katika miaka 50 iliyopita.
Akizungumzia
dira hiyo, alisema itakuwa ni ya nusu karne ijayo na malengo yake ni
kufikia mwaka 2061 chuo kitakuwa katika nafasi za juu za viwango vya
ubora vya kimataifa.
---
Habari via
Nipashe na
DHabariLeo