Tamko la vijana wa CHADEMA kuhusu mwelekeo wa Taifa na Chama
SUALA LA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU
Serikali imeshindwa kuendeleza elimu ya juu kinyume na ahadi zake. Hili linathibitishwa na mapungufu yafuatayo.
Mosi, Ilani ya CCM ya mwaka jana - 2005, iliahidi kuwa itawawezesha vijana wakitanzania wapatao elfu thelathini (30,000) kupata mikopo ya elimu ya juu kila mwaka. Kwa mujibu wa matokeo ya wanafunzi waliohitimu kidato cha sita mwaka jana, idadi ya wahitimu waliopata sifa za kujiunga vyuo vikuu ni takribani elfu ishirini. Tulitegemea kwa kuwa ahadi ya CCM ni kuingiza vyuoni wanafunzi elfu thelathini, basi, wanafunzi wote elfu ishirini waliokuwa na sifa wangepatiwa mikopo, lakini hilo halikufanyika.
Pili, mamia ya wanafunzi walirudishwa nyumbani kwa madai kuwa serikali haiwezi kuwapa mkopo ilhali walikuwa wameshaanza masomo. Kwa chuo kikuu “Mlimani” peke yake zaidi ya wanafunzi 300 walirudishwa nyumbani kwa kisingizio cha serikali kukosa pesa za kuwasomesha wakati walikwishapata nafasi za kusoma chuo kikuu na kuanza masomo.
Tatu, utaratibu uliotumika kuomba nafasi za masomo ya elimu ya juu na baadaye kuomba mkopo ulikuwa wa kutiliwa shaka kiasi cha kujenga mazingira ya serikali kuwalaghai vijana wake. Kabla ya matokeo ya kidato cha sita kutoka, vijana waliambiwa wanunue fomu za kujiunga na vyuo vikuu kwa madai kuwa kila atakayetimiza masharti ya kujiunga chuo kikuu atapatiwa mkopo. Katika hili vijana wengi wametapeliwa kwani kwa wale ambao hawakufikisha alama za kujiunga chuo kikuu tayari walikuwa wamepoteza elfu ishirini kwa kununua fomu kwa chuo kimoja, na wapo waliopoteza fedha nyingi zaidi kutokana na kuomba vyuo zaidi ya kimoja.
Nne, kulikuwa na gharama za kupata vyeti vya kuzaliwa ambazo vijana wengi hasa wa vijijini walilazimika kulipia ili kupata vyeti vyao na vya wazazi wao. Kulikuwa na gharama za kulipia fomu za mikopo 10,000/=, kusafirisha ama kusafiri kwenda vyuoni kuwasilisha fomu za kuomba mikopo na gharama kubwa za usumbufu wa kutimiza masharti ambayo ni pamoja na kugonga mihuri ya viongozi wa vijiji, kata na dini. Gharama hizi zikijumlishwa ni kubwa sana kwa watu masikini.
Tano, serikali ilibadilisha ghafla masharti ya mikopo. Awali, mikopo ilipaswa kutolewa kwa wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na vyuo vya elimu ya juu lakini, masharti yakabadilishwa kufanya wanaostahili mikopo kuwa ni wale wanaofayulu kwa kiwango cha daraja la kwanza “division one”wavulana na daraja la kwanza na la pili “division two” kwa wasichana.
Katika mchujo huo, vijana wengi waliokuwa na sifa za kujiunga vyuo vikuu walijikuta wakikosa mikopo na hatimaye kulazimika kurudi vijijini walikotoka. Kwa mara ya pili wanafunzi wakatapeliwa tena.
Sita, uamuzi wa serikali kuamua kuwa mkopo utakaotolewa kwa kila mwanafunzi ni asilimia 60 tu, na kwamba mwanafunzi anatakiwa kujilipia asilimia 40 zilizobaki ni mfano mwingine wa sheria kandamizi kwa vijana wanaotoka familia masikini. Kwa mzazi maskini aliyepata shida kumlipia kijana wake gharama za sekondari, gharama ambazo kwa wastani ni shilingi laki moja, haiyumkiniki aweze kumlipia kijana wake asilimia 40 ya gharama za chuo kikuu ambazo ni zaidi ya shilingi laki nne!
Vijana wa CHADEMA tunatoa mwito kwa vijana wote ambao kwa namna mmoja au nyingine walitapeliwa na serikali kuwasilisha malalamiko yao CHADEMA kwa ajili ya kuanza ufuatiliaji. Tunaahidi kushirikiana na vijana watakao jitokeza kuishinikiza serikali kwasababu tunaamini kuwa serikali inao uwezo wa kutosha kugharamia gharama za masomo kwa wanafunzi wote lakini yanakosekana mambo mawili;
Kwanza ni serikali kutokuwa na mkakati makini wa kuwasaidia vijana lakini pia kutokuwepo kwa jitihada za pamoja za vijana kuishinikiza serikali mpaka kieleweke. Katika hili, tunaiasa serikali iachane kabisa na mpango ilioutangaza wa kununua ndege nyingine ya rais, na badala yake fedha hizo zielekezwe kwa wanafunzi waliokosa mikopo ili wapate fursa ya elimu ya juu.
Pia, kwa kuwa mchakato wa kuandaa bajeti ya mwakani unaanza mara baada ya mwaka wa fedha wa sasa, tunaitaka serikali ihakikishe inatimiza ahadi yake ya kuhakikisha vijana 30,000 wanaingia chuokikuu, na waliopo wanapata mikopo kwa asilimia mia moja. Tunaitaka serikali itenge bilioni 195 kwaajili ya mikopo kwa wanafunzi wapya 30,000 na waliopo ambao ni takribani 35,000 wanaendelea kupata mikopo.